Kuna watu wengine ambao unakutana nao katika maisha halafu wanaishia kukupa hasira tu, unawaza hivi ni kwanini sikukutana nao miaka kadhaa kabla nakutana nao sasa, lakini yote ni mipango ya Mungu.
Miaka mitatu iliyopita nilikua katika kipindi cha kupigania ndoa, kipindi ambacho nililazimika kufanya vitu vingi vya ajabu ili tu mwanaume anikubali, nilikua nadhindani na wengi hivyo nikiamini kua mimi ndiyo napendwa zaidi nilijua nitaolewa mimi.
Lakini mpenzi wangu hakujali hilo, baada tu ya kunipata alinigeuza kama ka ATM kake, wote tulikua wafanyakazi wa serikali, alitaka kununua gari, hakua na pesa za kutosha na aliniomba nimkopeshe.
Nikiwa najua kabisa hatanilipa nilitoa kiakiba changu cha miaka miwili ambacho nilipanga kufungulia biashara na kumpa. Hiyo ilikua ni baada ya kumbembeleza na kumshauri sana kuwa kwanini afanye vile, kwanini tusingejenga kwanza.
Jibu lake lilikua yeye ni mwanaume siwezi kumpangia. Aliniambia kama nataka kumpanda kichwani wakati bado hajanioa akinioa itakuwaje? Niliufyata mkia nikanyamaza nikampa zile pesa lakini hata gari yenyewe hakununua, aliishia kuhonga Malaya wake.
Nilijua kwani walinipigia simu kunitukana kua mimi natafuta na wao wanahongwa, niliumia sana lakini baada ya kumaliza zile pesa basi alikuja kuniomba msamaha. Alijutia sana na kama unavyojua mwalimu wetu kipofu aliniambia msamehe, hakuna mwanadamu aliyakamilika.
Lakini sasa nilimpa mashariti kua tunapaswa kuwekeza katika maisha yetu, aliniambia anatafuta pesa anunue kiwanja na anataka kunioa. Kama kawaida ukisikia ndoa unchanganyikiwa, ingawa kwetu walikua wanamfahamu lakini sa alijitambulisha rasmi.
Alinivalisha pete ya uchumba kuonyesha kua alikua siriasi na mimi. Maisha yaliendelea na baada ya kuvalishwa pete nilivyokua mpumbavu nikageuka kua mke tena, nikijua kuwa nikikaa naye ndiyo nitamdhibiti nilihama kwangu na kwenda kuishi kwake, ndiyo ni upumbavu kuwa mke kabla hujaolewa.
Kabla hata sijaolewa basi tulianza kuishi pamoja nikiamini pete ndiyo cheti cha ndoa. Nilihamishia vitu vyangu kwake na tukawa mwili mmoja, hapo ndipo nilianza kuona chungu ya pilipili. Sio kwamba tu alizidi kuninyanyasa lakini alinipiga pia.
Akichelewa kurudi nikiuliza napigwa ananiuliza mimi ni Malaya tu kaniweka ndani na si mke. Lakini sinishavalishwa pete nilivumilia kwa wimbo uleule wa ndoa ni uvumilivu sijui hata nilikua navumilia nini wakati ndoa yenyewe hata sikua nayo.
Alinunua kiwanja kitu ambacho nilikua namshauri kila siku na akataka tuanze ujenzi, hapo nilijua mwanaume kabadilika, kwakua kipato chetu cha kawaida si unajua mishahara yetu hii basi aliniambia nichukue mkopo ili tukichanganya na kipato chake kidogo basi tujenge.
Nikijua kuwa tutakuja kufunga ndoa karibuni nilichukua mkopo, ujenzi ukaanza na Mungu si Athumani alijalia pamoja na vidilidili vyake vya kazini basi tulifanikiwa kumalizia ujenzi. Katika kipindi chote hicho tunajenga aligeuka na kua malaika, akiwahi kurudi na kufanya kila kitu kama mume mwema.
Lakini baada ya kumaliza kujenga, nikitaka kuhamia hapo ndipo ilizuka kasheshe. Wanaume ni washenzi ndugu zangu na hapa ndiyo najuta kwanini Kaka iddi sikukuona mapema nikasoma makala zako.
Unakumbuka makala moja ulisema kama mwanaume hajakuoa si mumeo chako ni chako na chake ni chake. Hilo ndiyo lilinitokea, nikijua najenga na mume wangu mtarajiwa kumbe nayeye alikua anajenga na mtu mwingine.
Yule mwanaume hakutumia hata senti tano katika lile jengo, alikua na mwanamke mwingine ambaye naye kama mimi alichukua mkopo tena wakwake wa benki kibiashara na kuwekeza kwenye ile nyumba. Lakini yule mchaga alinizidi kete, wakati mimi nasubiri kuambiwa tuhamie yeye alihamia kabisa.
Ndiyo kwa mbinde alianza kuishi pale kwenye ile nyumba, nilipotaka kwenda na mwanaume alikataa hakutaka twende, nilipokazania sana alinipiga na kunifukuza, ndiyo alinifukuza na kuniambia sina changu, nililazimika kuondoka na kwenda kuishi na rafiki yangu.
Wakati nikiwa huko nikagundua kua nina ujauzito wa wiki mbili, namuambia ananiambia hanijui. Yaani sijui nini kilitokea lakini nilisikia katangaza ndoa na yule mwanamke aliyekua akiishi naye, kabla hata sijastuka naambiwa wameoana ndoa ya kiserikali.
Ndiyo nikabakia na mimba yangu, yaani nilibaki nalia tu, nilitamani hata kujiua lakini maisha ilikua ni lazima yaendelee. Ilinibidi kuanza upya kwani mbali na ujauzito lakini mshahara mzima ulikua unaishia kulipa mkopo wa nyumba ambayo nilishanyang’anywa.
Mpaka leo hii nalipia mkopo na mpaka leo hii nawaona tu wakipita wapo na furaha na maisha yao. Yaani mimi nina mtoto wangu na wao yule mwanamke kumbe alishazaa naye mtoto mmoja mimi sijui na sasa ana mimba nyingine.
Natamani hata niende niichome moto ile nyumba kwani napata uchungu kila siku nikiangalia Salary Sleep yangu, kwa bahati mbaya wote tunaishi hapahapa Dar hivyo haiwezi pita wiki sijawaona.
Nina hasira sio kwasababu nimedhulumiwa tu bali nina hasira na wewe Kaka Iddi kwanini sikukujua mapema nikasoma makala zako mapema. Nina uhakika asilimia mia nisingefanya upuuzi nilioufanya. Kama unakumbuka tulishaongea niliponunua kitabu chako.
Nimeandika hivi ili wanawake wenzangu ambao wanabembelezea ndoa nao waamke na wasiwe mabwege kama mimi. Natamani hata kila siku uirudie ile makala yako kuwa kama mwanaume hajakuoa basi mali zake hazikuhusu.
Kuna wengi tu humu mnajifanya mnapendwa lakini siku likiwatokea mnawalaumu wahusika kumbe makosa ni yenu. Nimejifunza maisha yanaendelea ila nashukuru Mungu nilikupata kwani nilishakata tamaa, ila kwa ushauri wako kaka nimeanza biashara na inaenda vizuri.
Nashukuru kwa kitabu chako pia kimeniamsha sasa najielewa. Sipo kwenye ndoa wala mahusiano kwa sasa ila najua kabisa kuhusu wanaume, nimejifunza mengi kupitia makala zako na zaidi katika kitabu chako, kaka umeniponya.
Sasa hivi nataka kulipa kisasi, sitaki kulipa kisasi cha kuchoma nyumba yao moto bali cha kujenga nyumba yangu na kufanikiwa zaidi. Nakumbuka siku ya mwisho tulipoongea uliniambia hakuna kisasi kizuri kama kua na furaha zaidi ya mtu aliyekuumiza kumuonyesha kuwa humhitaji yeye kufurahi Ahsante kaka bray.
***
#SHARE KUNA WANAWAKE WENGI BADO WAMELALA
#SHARE KUNA WANAWAKE WENGI BADO WAMELALA