WATAALAM wa masuala ya mapenzi wanaeleza kuwa, unapokuwa katika uhusiano na mtu uliyetokea kumpenda sana, usimkabidhi moyo wako wote kwanza.
Chukua muda wa kumchunguza ili kubaini kama na yeye pia anakupenda kwa dhati kutoka moyoni mwake ama laa. Ukishabaini naye anakupenda, nawe mkabidhi moyo wako kisha yafurahieni maisha yenu. Lakini ukiona moyo wako unasita kuendelea kuwa na mtu huyo na kuhisi hana penzi la kweli, ni vizuri bila kujali jinsi utakavyoumia ukamuacha haraka kabla ya yeye kukuacha.
Kumuacha kwako kutakufanya uwe na amani moyoni mwako kwani utakuwa umejiandaa kumkosa mwenyewe kuliko yeye kuja kukuacha ghafla, utaumia na unaweza hata kuzimia pale atakapokuambia wewe na yeye basi. Nalazimika kuandika makala haya kwa kuwa, unamkuta mtu anaumizwa kila wakati na mpenzi wake lakini kwa sababu tu anampenda, anaamua kuvumilia huku akiamini kwamba ipo siku penzi lao litatengemaa.
Kimsingi hutakiwi kulilea penzi lisilokuwa na muelekeo, usikubali kulizwa, unapoona nyendo za mpenzi wako hazikuridhishi, chukua uamuzi wa haraka wa kumuacha huku ukiamini kwamba utampata mwingine.
Kimsingi mtu asiye na penzi la kweli, utamgundua tu. Kwa mfano mpenzi wako anakuwa mgumu wa kuonana na wewe, mawasiliano duni, msiri sana, hakujali, haoni hatari kukueleza kwamba muachane, haoneshi kukupenda kiivyo, huyu ipo siku atakuacha na kukuumiza sana.
Sasa kwa nini usichukue hatua za haraka za kumtosa? Kuna raha gani ya kuwa na uhusiano na mtu asiyekupa raha ya maisha badala yake ni mtu wa kukufanya uwe na majonzi kila wakati?
Usikubali kuwa mtumwa wa mapenzi kwa kukubali kuburuzwa na mtu unayeweza kumuacha na maisha yako yakaendelea kuwepo. Amini wewe ni mzuri, handsome na una kila kigezo cha kupata penzi la uhakika na si la kubabaisha.
Baada ya kusema hayo nikupe dondoo mbili tatu zitakazokusaidia pale itakapotokea umeachwa na mpenzi wako wakati bado unampenda. Kwanza yakumbuke mabaya yake yote aliyowahi kukutendea. Wapo wengi wameachwa na wapenzi wao lakini maisha yao bado yameendelea kuwa mazuri na ya furaha.
Walichokifanya ni kujaribu kusahau yale mazuri waliyokuwa wakifanyiwa na wapenzi wao na kuyakumbuka mabaya waliyokuwa wanatendewa.
Kingine jitahidi sana kutoonana naye mara kwa mara. Ni ukweli ulio wazi kwamba, utakapokuwa unaonana na mpenzi wako wa zamani ambaye ulikuwa ukimpenda utakuwa unaumia sana. Kwa maana hiyo jaribu kuepuka kuonana naye ili kujiondoshea maumivu.
Lakini, hata kama kakuumiza vipi, huwezi jua sababu ya yeye kukuacha kwani kila kinachotokea hapa ulimwenguni kimepangwa na Mungu. Hivyo basi, kama ulikuwa unamheshimu endelea kumheshimu, msalimie pale unapoonana naye na hata pale atakapokuwa anahitaji msaada wako, msaidie.
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo unatakiwa kuyazingatia pale utakapoamua kumuacha mtu ambaye ulikuwa unampenda sana lakini yeye akakutenda.