Ndugu zangu maisha ya mahusiano yanahitaji faraja. Mahusiano yanahitaji utulivu; mioyo yenu itulie ili muweze kufanya mambo ya kimaendeleo. Wengi wamejikuta wakisuasua katika kufanya maendeleo kwa sababu tu ya kuyumba kimahusiano.
Mahusiano yanapokuwa na shida basi husababisha mambo mengi yasiende sawa. Ni vizuri sana wapendanao wakahakikisha wanaitafuta kwa gharama yoyote. Kila mmoja aone ana wajibu wa kulinda furaha ya mwenzake, mkiishi hivyo basi hakika mtainjoi maisha.
TURUDI KATIKA MADA
Nikirudi kwenye mada yangu ya leo, nimedhamiria kuzungumza nanyi kuhusu umuhimu wa kuheshimu ulipo. Vijana wengi siku hizi wapo njia panda kwa kushindwa kung’amua yupi hasa ni mwenza sahihi wa maisha. Leo mtu anakuwa na huyu, anaishi naye kwa miezi miwili mitatu anahamia kwa mtu mwingine baada ya kuhisi labda hawaendani na mtu husika. Hii ni changamoto kubwa, hakuna mtihani mkubwa kwa vijana kama huu.
Kumpata mwenza sahihi wa maisha ni kama vile mtihani wa maisha. Ukifanya vibaya kwa maana ya kuchagua basi utapata matokeo mabaya. Wengi huangalia sana matamanio ya mwili na sio tabia. Mwanamke anahangaika na kijana handsome, anataka awaringishie marafiki zake kwa kuwa na kijana mzuri. Vivyo hivyo kwa wanaume, nao wanahadaika na uzuri wa sura za wanawake. Matokeo yake wanajikuta wakisuasua katika suala zima kupata mwenza sahihi wa maisha. Matokeo yake hujikuta wamepoteza muda. Ndugu zangu, kwenye maisha ya mahusiano unatakiwa kuwa na msimamo. Unatakiwa kujua nini unatakiwa kufanya na kwa wakati gani ili kuepuka kujutia muda.
JIRIDHISHE KWANZA
Kabla ya kuanzisha uhusiano na mwenza wako hakikisha tu kwanza umejiridhisha. Umjue angalau anaishije, ni mtu wa aina gani? Ni mtu mwenye heshima, anayejitambua? Kuna baadhi ya watu ukiwaangalia tu katika hatua za awali unaona kabisa hawafai. Unamuona ni mtu mkorofi, ni mtu mhuni ambaye hapendi hata umjue kiundani. Mtu wa aina hiyo unapomuona ukiwa katika hatua za awali ni vyema ukamuepuka na ukasubiri au kutafuta mtu ambaye ni sahihi.
UKISHAJIRIDHISHA…
Ukishahakikisha kwamba upo na mtu sahihi, angalau si kila kitu basi unachotakiwa ni kuwa na msimamo. Hakuna mtu ambaye hana mapungufu. Kila binadamu ana mapungufu yake hivyo kikubwa kinachotakiwa ni uvumilivu. Mvumilie kwa kila hali. Yawezekana akawa na matatizo fulanifulani katika kuzungumza au namna ambavyo anakuchukulia wewe kama mtu wake lakini huna budi kumvumilia. Mpe nafasi pia ya kubadilika maana kuna baadhi ya mambo mtu anaweza akabadilika kulingana na jinsi mnavyoishi.
ULIPO NI BORA
Amini kwamba ulipo ni salama zaidi kuliko kule ambako unataka kwenda. Uliye naye ni bora kuliko ambaye bado hujakutana naye. Mheshimu, mthamini maana huyo angalau unamjua kidogo. Komaa naye, kubali kukua naye na mtafanikiwa.
Usiwe mwepesi wa kukata tamaa ya kuhamia mara kwa huyu mara kwa mwingine, kaa na mmoja jipe nafasi ya kujifunza kutoka kwake naye ajifunze kutoka kwako. Itafika mahali mtakuwa mmezoeana na mnajuana vizuri.