Nilijua kama akinioa atabadilika, nilikaa kimya kila siku aliponipiga sikuongea wala kujibu chochote kwani kila mara nikiongea alikua akiniambia kama nimechoka niondoke na nilipomuambia simtaki tena alikuja kuniomba msamaha. Nilipomsamehe alirudia yaleyale, nilichoka na kuondoka lakini sijui kwanini bado kwa ujinga wangu nilirudi.
Kumbuka hapo alikua mpenzi wangu tu lakini alikua akinipiga kama vile ananimiliki. “Mwanangu ana hasira za karibu, mvumilie tu! Sasa wewe nawe ukimuacha unafikiri atapata wapi mwanamke mwingine wa kumuoa!” Mara kwa mara Mama yake aliniambia pale nilipotaka kumuacha mwanae.
Sio mimi nilikua nikimuambia, hapana, ila kila mara nikigombana na Juma alimuambia Mama yake kuongea na mimi. Nakumbuka kipindi hicho nilikua na mimba yake ya miezi mitano, alikua bado hajanioa, tulikua hatuishi pamoja lakini muda mwingi alikua akiutumia kwangu. Nilikua nimechelewa kutoka kazini, kulikua na kikao ofisini na mimi kama mwandishiwa vikao ilikua ni lazima niwepo.
Alikua anaijua kazi yangu lakini alifanya makusudi tu kwanini nimechelewa na kwanini nililetwa na Gari ya Bosi. Akilazimisha kwanini nisingechukua Bodaboda, alishindwa kuniamini nilipomuambia kuwa sio mimi peke yangu nilipelekwa na Gari, wafanyakazi wote tuliochelewa siku ile tulipelekwa na Gari ya Bosi.
Aliniambia kama nampenda kweli niache kazi lakini nilipokataa basi alianza kunipiga bila kujali hali yangu. Kidogo mimba itoke lakini nashukuru Mungu siku ilipita salama. Alinipiga sana na nilimuambia basi, nilitaka kwenda Polisi ndipo alimpigia simu Mama yake ambaye alinituliza akiniambia maneno ya kuonyesha dhahiri alikua upande wa mwanae.
Baada ya hapo nilijikuta na mchukia tu, mwanzoni alikua akinipiga bado nampenda, najipendekeza kwake lakini baada ya kunipiga nikiwa na mimba mapenzi yaliisha kabisa na nilianza kumuona kama takataka flani. Alijitahidi kuniomba msamaha lakini wapi, sikutamani hata kusikia sauti yake, nilishatoa mimba zake nne wakati wote akiniambia hataki kuzaa na mimi.
Hii ya tano sikua tayari kutoa nilijua kufanya hivyo ningeweza hata kupoteza kizazi. Baada ya kuona sina uchangamfu wa kama awali aliniacha, akaendelea na umalaya wake, akitembea na kila rafiki yangu na kila mtu niliyekua namfahamu, mimi sikujali na kwakua nilikua na kazi yangu sikutaka hata kumsumbua.
Hata nilipojifungua alisema hawezi kuja kumuona mtoto, alikua akisingizia si wake lakini kwa mtu aliyemuona pamoja na kuwa alikua wakike lakini alichukua sura yake kama kopi vile. Mama yake alimsihi sana anisamehe turudiane lakini hakua tayari na mimi sikujua hata alitakiwa kunisamehe nini wakati kila siku ndiyo alikua ananikosea kwa kunipiga bila sababu.
Miaka miwili ilipita bila kuja kumuona mtoto, nilianza kuendelea na maisha yangu na nilipata mtu mwingine ambaye alinipenda mimi na mwanangu, alikua akinijali na kunipa kila kitu. Hapo ndipo nilimuona akirudi, alianza kunitafuta akiniambia kuwa hataki mtoto wake alelewe na mwanaume mwingine, aliniomba msamaha na kunisumbua kila siku.
Sikutaka kumsikiliza lakini naye hakutaka kukata tamaa, bila hata kuongea na mimi alituma wazee wake kwetu, kuja kuongea kuhusu ndoa. Alileta posa hata bila mimi kujua, hapo nilianza kuhisi kua labda kweli kabadilika ananipenda hivyo kwa kumuangalia na mtoto niliachana na mpenzi wangu ambaye alikua ananipenda sana na kukubali kuolewa nayeye.
Kweli mambo yalienda vizuri, miezi mitatu ya kwanza ilikua ni ya amani sana, alionyesha kunipenda na kuficha wivu wake. Lakini nilipata ujauzito wapili, hapo ndipo mambo yalibadilika, alitaka niache kazi nilee watoto kwa kisingizio pesa ninayopata ni ndogo hivyo ni kama naenda kufanya umalaya tu huko kazini.
Sikumuelewa niligoma kabisa, hapo ndipo alianza kukasirika, kuchelewa kurudi na kunipiga kukawa palepale. Siku moja kulikua na kikao, nakumbuka kilikua ni kikao cha kamati ya fedha hivyo mimi kama CC nilipaswa kukaa mpaka mwisho. Nilimpigia simu kua kuna kikao lakini alikataa kiniambia nirudi nyumbani na kama ikifika saa mbili sijarudi basi nisirudi tena kwake.
Kusema kweli nilichanganyikiwa kwani kwa hali niliyokua naiona kingefika hata saa nne usiku. Nilimtumia meseji tu kua kikao kikiisha nitarudi kisha nikaendelea na kikao. Usiku kwenye saa nne hivi kikao kikiendelea, nilisikia mngurumo wa gari, mara gari likasimama na nnje nilisikia mzozo kati ya mlinzi na yeye.
Alikua akilazimishia kuingia kwenye kikao kunichukua, alikua akipiga kelele kusema namtaka mke wangu namtaka mke wangu! Nilijua anataka kuniaibisha, harakaharaka nilimfuata Afisa Utumishi nikamuomba kutoka nikimkabidhi makabrasha ya kuandikia mihtasari. Nilitoka kumfuata na kabla ya kusema chochote alianza kunipiga, alinipiga sana aakaniingiza kwenye gari na kunipeleka nyumbani.
Huko alinipiga na mikanda, mateke ya kila sehemu bila kujali kama nilikua na mimba yake au mtoto alikua anaona. Alinipiga sana kisha kunifungia jikoni. Nilikaa huko nikipata mauivu makali mwilini, niliumia sana mpaka kupoteza fahamu, hakurudi mpaka asubuhi, alirudi na kunifungulia akijifanya kukasirika.
Alianza kulalamika kuwa tabia zangu ndiyo zinamfanya kunipiga na kumpandisha hasira zake za karibu. Sikusema chochote ziadi ya kuomba msamaha ili nisipigwe tena. Alijifanya kukubali na kuniambia niamke nikamuandalie Chai. Nilijaribu kunyanyuka lakini nilishindwa, nilikua siisikii miguu yangu.
Yeye aliona kama kiburi mpaka aliponishika kuninyanyua lakini nilikua mzito, mwili hauna nguvu, na wala sikua na maumivu yoyote kuanzia kiunoni kushuka chini. Alijaribu kuninyanyua tena na tena lakini wapi. Sikujua kinachoendelea lakini nahisi yeye alihisi kitu kwani alininyanyua na kunipeleka kwenye gari.
Alinichukua na kunipeleka Hospitalini, kule alisema kuwa nimeanguka kwenye ngazi lakini Daktari hakuamini, ila sijui alifanya nini nikaanza kutibiwa hivyo hivyo bila PF3. Hapo ndipo nilipewa habari mbaya, nilikua nimevunjika sehemu ya uti wa mgongo na nisingeweza kutembea tena katika maisha yangu.
Kwangu ilikua ni kama msiba, nilishindwa kuamini lakini ilikua hivyo, ndugu zangu walikasirika na kukasirika lakini haikusaidia. Walitaka kumpeleka Polisi lakini nilikataa nikiwaambia haitanisaidia kutembea. Nilikaa Hospitalini kama mwezi mmoja hivi kuona kama kutakua na mabadiliko lakini wapi, ilikua hivyo nilishakua mlemavu na ilibidi tu kukubaliana na hali yangu.
Nilirudi nyumbani na kuwa mtu wa kusaidiwa kila kitu. Mwezi mmoja tu baada ya mimi kutoka Hospitalini aliniambia anataka kunirudisha kwetu kwani yeye hawezi kunihudumia tena, hawezi kuishi na mwanamke mlemavu, nilijaribu kumuambia yeye ndiyo kanisababishia lakini alisema haitasiadia, hata kama ni yeye lakini hawezi kuishi na mimi tena.
Nilijua utani lakini alileta mwanamke mwingine nikiwa mulemule ndani na siku iliyofuata alinichukua na kuja kunitelekeza kwa Mama yangu na mwanangu, mimba ile ilishatoka siku aliponipiga. Ni mwaka sasa hajapiga hata simu ya kunijulia hali, pesa ya matumizi ya mtoto anatuma tu kwa simu hata kuongea na mtoto hawezi.
Sasa hivi nipo tu nyumbani sina kazi sina hili wala lile naishi tu na Mama yangu ambaye naye ni mzee naona anavyppata shida kunihudumia. Nimeandika kisa changu ili wanawake wenzangu mjifunze, mimi yameshatokea siwezi badilisha kitu ila kwako wewe ambaye unapigwa na unaona kama ni kitu cha kawaida unaweza kuabdilika sasa.
Unaona kama ana hasira za karibu nikuambie tu kuwa hana haki ya kukupiga na wewe si lazima kuvumilia mateso. Nibora kuondoka ukiwa na miguu yako miwili na nguvu zako kuliko kusubiri mpaka hali ikufike kama mimi. Nilijipa moyo atabadilika nasikia kabadilika kweli mkewe mpya hampigi lakini mimi nimepata faida gani ya kubadilika kwake?
Najua umenielewa sidhani kama utaendelea kuvumilia kupigwa ukisubiri kuwa mlemavu kama mimi!
****MWISHO;