Wewe ambaye umeoa au kuolewa na upo unafikiria kuachana na mwenzi wako.
Fikiria upya uamuzi wako.
Fikiria hao watoto mlionao, Fikiria nyakati zote nzuri mlizokuwa nazo pamoja kama mke na mume, Fikiria sehemu tofauti ambazo mlitembelea pamoja, marafiki wazuri mliokuwa nao wote wawili kama mke na mume.
Iepuke talaka kwa gharama zote, sababu zinazokufanya uamue kuachana na huyo mume wako au mke wako zinaweza kuwa ndizo zitakazokuwa sababu mara nyingine tena mbele ya safari kama utaamua kuoa au kuolewa tena.
Sasa unaachana na Jimmy kwa kuwa umechoka na tabia zake za kulewa sana pombe, au kukutaka sex mara nne kwa siku na next time unaweza kujikuta unaachana na John kwa kuwa anakupiga mingumi usiku kucha na yeye sex kwa mwaka mara moja.
Inawezekana unataka kuachana na mary kwa sababu ni msumbufu na anakusema hata kwa vitu vidogo, hata hivyo unaweza kujikuta unaacha na Joyce baadae kwa sababu si mwaminifu katika fedha.
Sasa utaishia wapi na hiyo project ya kuachana na kila unayeoana naye?
Ukiangalia kwa makini kinachobadilika ni tabia na mhusika tu ila wote ni binadamu na binadamu asiye na kasoro bado hajazaliwa hadi leo.
Maisha ni matamu sana kiasi cha kuyapoteza kwa kupeana talaka.
Wanaume wote duniani wanafanana pia wanawake wote duniani wanafanana , na sote ni binadamu.
Wapo wanandoa ni wazembe kiasi ambacho huacha kutumia kila alichonacho kuhakikisha ndoa inarudi kwenye mstari, kukimbilia talaka si jibu bali ni kusukuma tatizo mbele na matokeo yake utakuja kukutana nalo tena mbele ya safari.
Hata kama kuna mtu amekuahidi kwamba ukiachana na huyo uliyenaye basi yeye atakufanya uwe mtu mwenye furaha, hatakuumiza wala kukuacha, ni mwongo na anakudanganya kwani katoka sayari gani na binadamu gani.
Anaonekana anakufaa kwa kuwa huishi naye ukianza kuishi naye utajikuta umeruka mikojo.
Jiulize mwenyewe upya.
Hivi kweli nimetumia uwezo kiasi gani kuhakikisha mwenzi wangu anajua namna tunahitaji kuirudisha ndoa yetu kwenye mapenzi upya kama tulivyoahidiana siku tunaoana?
Je, ni kweli nimefanya kila linalowezekana kusamehe na kusahau?
Je, ni kweli tunataka kuachana na kupeana talaka kwa sababu za msingi?
Kabla ya kuwasiliana na ndugu zako, rafiki zako, washauri wako, wanasheria au wachungaji wako Jaribu kukaa mwenyewe, na mwenzako kujadili upya na kwa upendo namna ya kutatua tatizo lenu na hakuna anayejua shida ya ndoa yako isipokuwa wewe na mwenzi wako.
Usifanye uamuzi wa kuachana kwa haraka ukiamini unaingia kwenye uhuru.
Dawa ya kuachana au talaka ni kusamehe bila masharti.