Nilikuwa kwenye daladala siku za karibuni na nikawasikia wasichana fulani wawili wakimsema rafiki yao mmoja ambaye alikuwa ameachwa na mpenzi wake.
Walikuwa wakionyesha kumuonea huruma kabla ya mmoja wao kusema kwamba, rafiki yao huwa anaachika kwa sababu ya sura yake.
Walikumbushana namna rafiki yao huyo alivyokuwa akiachwa na wakakubaliana kwamba, iwapo asingekuwa na sura nzuri sana basi huenda angekuwa na bahati zaidi.
Nilipokuwa nateremka kituoni, nilianza kuwaza kuwa walichokuwa wanasema juu ya uzuri wa mtu na kuachana katika mapenzi kinakaribiana na ukweli.
Na hilo lilinifanya nifanye utafiti mdogo na kufanya hitimisho langu binafsi. Nilichogundua, kilinipa sababu zifuatazo;
Wazuri huwavutia watu wengi sana ambao hujaribu kufanya kila liwezekanalo kuwa nao. Hata kama wakiwa kwenye mahusiano, watu hawa huwa na watu wengine pembeni ambao kila mara wanakuwa wanataka kuwatoa, au kuwatania kimapenzi na kadhalika.
Hili linawaweka wapenzi wao katika hali ambayo wanahisi penzi lao kutokuwa salama. Wanahisi kuwa, wapenzi wao wazuri wanawavutia watu wengi kiasi kwamba wanashindwa kuwa na muda wa kutosha nao. Hili mara nyingi husababisha mahusiano kuvunjika.
Wasichana wazuri, hata wanaume wanajiona kuwa wao ndiyo wao kutokana na kuwavuta watu wengine wa jinsia tofauti.
Ni jambo la kawaida kwa mtu kupata kichwa hasa pale kutokana na mawazo ya watu. Kwa watu wazuri na wanaovutia sana, kikubwa wanachosikia kutoka kwa watu wengine ni jinsi walivyo pendeza na mambo kama hayo.
Baada ya muda, mtu anaanza kupata kichwa na wanaanza kujidhania kuwa wao ni bora kuliko mtu mwingine yeyote. Iwapo hili litatokea katika mahusiano, yule mzuri na anayevutia anaweza kuanza kumwona mwenzake kama hamsahili na hivyo kuamua kuachana nae au yeye kuachwa.
Mahusiano ni jambo la pande zote ambapo wote wanafanya jitihada ili mahusiano hayo yaweze kufanikiwa. Utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa, watu wanaovutia zaidi hawajali sana juu ya mahusiano yao hivyo hawaweki nguvu yoyote ili ufanikiwe ukilinganisha na wenzi wao. Mara nyingi, wanaamini kwamba uzuri wao unatosha kuwa na huyo mwenza. Iwapo mwenza anapoanza kuhisi kwamba anafanya zaidi katika mahusiano hayo, wanaweza kuchoka na kuamua kubwaga manyanga.
Katika mahusiano mengine, wenza kwa wazuri wanaweza kuanza kujihisi hawatoshi au hawastahili baada ya muda fulani. Wanakuwa sehemu na wenza wao wazuri na wanasikia wakisifiwa kutoka kila mahali, hivyo hili linaweza kuwafanya kuhisi kuwa wapo na mtu ambaye yupo ‘standard’ ya juu zaidi yao. Matokeo ya hili ni kujaribu kudharau sifa za nje na kupeleka nguvu katika kufanya mahusiano yaende vizuri lakini wengi hushindwa na wengi huamua kuchukua njia rahisi, kuachana.
Ni hulka ya binadamu kutaka kuwa na mtu mzuri kama mwenza. Wengi huingia kwenye mahusiano na watu wazuri kwa lengo la kuwaonyesha watu. Hii ina maana kwamba, msichana mrembo anaweza kuingia kwenye mahusiano na mwanaume ambaye lengo lake hasa ni kupata sifa kwa kupitia yeye. Hili linapofanikiwa, anaweza kuamua kuendelea kuwa na msichana au kumuacha. Akiamua kumuacha, msichana ataumia kwa uongo wa huyo mwanaume. Hii ni kwa sababu, wazuri wana watu wengi sana katika jamii kwa sababu nyingi zisizofaa.
Wazuri mara nyingi huwa ni wahanga wa kupokea sifa nyingi mno. Mtu anapozoea sifa kutoka kila upande wa dunia, wanaanza kuzitegemea kwa ajili ya kuishi. Mtu huyu anapokuwa kwenye mahusiano, sifa huenda zikaanza kupungua, kwa kuwa watu wanajua kwamba huyo mtu hayupo sokoni kwa wakati huo. Hili linaweza kumfanya mzuri kuhisi kupungukiwa kwa kuwa anashindwa kupata ‘chakula’ cha kutosha kutoka kwa mwenzi wake. Kutokana na hali hii, wanaweza kuamua kuacha au kuachwa kwa kujaribu kuonekana na watu wengine.
Mtu anapokuwa na uchaguzi mpana sana, uchaguzi unachukua muda mwingi. Na inawezekana usiwe ni uchaguzi wa mwisho kwa sababu mtu huyo anaweza kutumia njia ya majaribio. Hili ni jambo la kawaida kwa wazuri, wanakuwa na wengi wanaotaka kutoka nao hivyo wanashindwa kuchagua. Anapoanza kutoka na huyu, anaweza kumwona mtu mwingine ambaye angependa kumjaribu na anaweza asiache kujaribu. Hili linaweza kusababisha kuwa na mahusiano mengi ya muda mfupi.
Katika mazingira mengine, wazuri wengi hutumia uzuri wao kupata nafasi, ikiwemo katika mahusiano. Hili linamaanisha kwamba, wakati mwingine wanaweza kuingia kwenye mahusiano bila kuwa na kitu kingine kuleta kwenye mahusiano haya zaidi ya uzuri wao. Kama Benedict Beckeld alivyowahi kusema, watu wazuri ni mara chache sana kutaka kutafuta digrii za juu, au kujifunza lugha mbalimbali. Iwapo ndivyo hili lilivyo, mtu aliye nao anaweza kuchoka kwa kuwa hana anachopata kutoka kwao zaidi ya uzuri. Mara nyingi, mahusiano ya aina hii huishia kwenye kuachana.
Baada ya kusema hayo, naweza kuungana na wasichana wale kwenye daladala na kusema kuwa inawezekana rafiki yao aliachwa kwa kuwa mzuri mno. Naweza pia kusema sifahamu hasa ni wakati gani mtu anaweza kuitwa mzuri sana au hapana, nasikia kuwa uzuri upo kwenye macho ya mtu.