Katika maisha ya sasa hivi wakati mwingine inakua vigumu sana kuepuka mwanao kulelewa na Mama wa kambo, hii inatokana na ukweli kuwa watu wengi huzaa kabla ya ndoa na wengi hutengana hivyo kuna wakati Baba atataka kuishi na mtoto na anaweza kuwa ameoa au anaishi na mwanamke hivyo kulazimisha mwanao kulelewa na Mama wa kambo. Si kitu kibaya na niseme tu kuna Mama wa kambo wengi wenye roho nzuri.
Kama wewe ni mfuatiliaji mzuri wa ukurasa wangu huu wiki iliyopita niliandika stori kuhusu mtoto aliyekua akinyanyaswa na kuteswa na Mama yake wa kambo, ilikua ni stori ya kweli ambayo ilimtokea mmoja wa wasomaji wangu. Mara nyingi wanaume wanakua bize na kazi, hawana muda na watoto, hivyo mtoto anaweza kuteseka lakini Baba asijue anateseka au kutokana na mapenzi basi hata akiambiwa akwa hasikii.
Lakini wakati mwingine anaweza kuwa akiambiwa ila kwa kutaka kumkomoa Mama wa mtoto, labda alimuacha vibaya akaamua kukaa kimya au anaweza kuambiwa lakini akawa anajiambia kuwa labda ni kwakua Mama wa mtoto bado anampenda hivyo anasingizia ili aachane na mkewe. Sasa nimeulizwa swali hili mara nyingi, kuna wamama wengi wana wasiwasi baada ya kusoma kile kisa hivyo kama mwanao analelewa na Mama wa kambo hembu fanya yafuatayo;
(1) Acha Kushindana Na Mama Mlezi/Muache Awe Na Amani; Kuna wanawake wengi ambao hawakubali kuachika, wanakua na vidomodomo na kila mara hawataki kuwaacha watu kuwa na amani. Inawezekana uliachwa vibaya, labda huyo mke mpya alikunyang’anya mwanaume tena kwa dharau. Lakini kumbuka ushaachwa, hurudiwi hivyo badala ya kupoteza muda wako kutaka kumharibia nayeye hembu endelea na maisha yako.
Kuna wanawake huwatumia watoto kama fimbo, kwakua tu anaishi kwa Baba yake unapiga simu mpaka usiku, saa nane usiku unapiga simu kuulizia hali ya mtoto. Lakini haiishii hapo, unaenda kutembelea unatukana, unakosoa kila kitu, unamsengenya na kama ukute wewe ndiyo unapendwa na ndugu basi kila siku ni kupiga simu kwa mawifi kumsema ubaya, kama hana mtoto ndiyo tena unatukana mpaka basi.
Nikupe tu taarifa kuwa kama unamfanyia mabaya kudhani unamkomoa wakati anakulelea wanao basi wewe ni fala na nadhani hujielewi kwani yule ni binadamu, anaweza kuchukiwa na mume, akachukiwa na ndugu akawa na hasira ila zote zitaishia kwa mwanao! Hata kama ni mwema kiasi gani lakini jinsi unavyompa machungu jua unamsukuma kumchukia mwanao, hivyo kabla sijakuambia mengine ya kufanya hakikisha unamuacha kwa amani.
Si watetei lakini kama wewe ni kisirani kwake basi jua nayeye atakua kisirani kwa mwanao. Halafu nikuambie tu yalishakushinda, kuna sababu uliachwa, najua unajiambia kampa dawa, au kamteka kimpenzi sijui na nini lakini ukweli nikuwa umeachwa hivyo pambana na hali yako. Hembu kuwa na amani, wewe si wa kwanza kuachwa, usimlazimishe kumchukia mwanao kwani anaweza kulipia kisasi kwake akateseka wee wakati yeye wala humuumizwi kichwa na maneno yako!
(2) Ongea Na Mwanao Kijanja; Wanawake wengi wakiwa katika hali hii wanapenda kutafuta makosa, kwa maana hiyo watawauliza watoto mambo mabaya ambayo hufanyiwa na Mama zao wa kambo. Hii ni kwasababu wanaamini kuwa yapo hivyo ni kama wanataka ushahidi, inawezekana ushamchukia huyo mwanamke. Hivyo utakuta anauliza “Anakupiga? Anakunyima chakula? Anakufanyisha kazi nyingi?”
Mtoto anayenyanyaswa tayari kashaogopeshwa, ashatishiwa hivyo kamwe hawezi kusema kuwa anapigwa, ananyanyaswa na vitu kama hivyo. Wapo wachache husema lakini wengi huogopa kuwa wakisema huyo Mama atajua hivyo kuongezewa mateso hukaa kimya au kusema hapana. Sasa unatakiwa kuulizaje? Uliza kijanja, kwa mfano unataka kujua kama ananyimwa chakula.
Badala ya kumuuliza “Uanyimwa chakula?” Mulize “Jana mlikula chakula gani?” atakuambia kisha mjibu “Na Baba naye alikula… Mama naye alikula nini Na Flani (jina la mtoto wa huyo Mama yake wa kambo) naye anapenda kitu flani kama wewe?” Hapa mtoto atajikuta anasema chakula aliichokula yeye. Mfano kama ananyimwa au hali sawa na wengine utasikia “Mimi nilikula ugali, Baba yeye hali na sisi wanakula sebuleni na Mama, Flani alikula…”
Hapa kutokana na majibu utajua kuwa kumbe chakula nacho wanakula tofauti! Au kama akikuambia alikula ugali ukamuuliza “Mbona unapenda ugali sana?” kama ananyanyaswa utasikia “Mama ndiyo anasema nile ugali… mimi napenda..” Ukamuuliza kama alishiba. Badala ya kumuuliza kama anapigwa ukamuuliza “Mimi na Mama yako flani nani mkali?” Hapo anaweza kukuambia ukali wake namna anavyopigwa na vitu kama hivyo.
Badala ya kumuuliza kama anakatazwa kuangalia TV ukamuuliza “Wanalala saa ngapi?” Anapenda mchezo gani katika TV. Badala ya kumuuliza kama anaamshwa asubuhi kufanya mikazi ukamuuliza anaamkaga saa ngapi, au nani anamuamsha. Kwakifupi usimuulize mwanao swali la moja kwa moja ambalo anajua akitoa jibu ni kama kumshitaki Mama yake wa kambo, hatasema kwani anaogopa kupigwa kashatishiwa hivyo uliza kijanja janja.
(3) Mkague Mwanao; Hakikisha unamuona mwanao hata mara moja kila baada ya miezi sita kama mnaishi mbali sana. Kama ni karibu hata kwa mwezi mara mbili hakikisha unaonana naye. Unapokutana naye hembu mkague, watoto wengi wanaonyanyaswa hasa kwa kupigwa huwa wanakua na makovu sehemu za siri na mgongoni, hizi ni sehemu ambazo mtesaji anajua watu hasa Bbaa yao hataziona.
Mkague mwanao, hata kama ni mkubwa, usimuambie unamkagua hapana, angalia bila yeye kujua unaangalia, unaweza kujifanya unambadilsiha nguo, unamuogesha na fanya kitu chochote kile umkague. Ukikutana na makovu usipaniki, uliza kijanja na usisikilize majibu yake soma sura yake wakati anakujibu. Inawezekana kashaambiwa cha kusema kwamba akiulizwa aseme alidondoka au kapigwa shuleni hivyo angalia uso wake.
Mtoto anayenyanyaswa unapoona vidonda vya mateso basi hunywea, huanza kuona aibu tofauti na vidonda vya shuleni. Kama ni kupigana shuleni huona kama ni ufahari, hujiona kama ni shujaa hivyo hata hatavificha, lakini kama ni vile vya kunyanyaswa iwe ni shuleni au Mama yake wa kambo basi huogopa kuvionyesha, huona aibu na anakua anafichaficha, hivyo sikiliza majibu na ukiangalia sura yake.
(4) Ongea Na Baba Yake, Usilalamike; Kuna kitu ambacho wanawake wengi hukosea na kusababisha watoto wao kuendelea kuteseka kila siku. Umegundua na una uhakika kabisa kuwa mwanao anateseka, iwe kwa kuchunguza na hata kuambiwa, unachukua simu unampigia Baba yake, unaanza kutukana au unapaniki, unaanza kumdai mwanao sijui na vitu gani.
“Namtaka mwanangu, sijashindwa kumlea, huyo Malaya wako atanitambua…” Unatukana mpaka basi! Inawezekana labda hutukani, lakini unalalamika, unaanza kuongea “Ohhh mbona anamfanyia hivi mwanangu…mtoto hali…mtoto hivi na vile…” Unalalamika wee mpaka basi. Hapa mwanaume hatakusikiliza, atajua ni wivu wa kike na unamtumia mwanao kumuumiza mke wake.
Hatachukulia maanani kama kila siku utakua unalalmaika au kutukana na kutoa vitisho. Hembu ukikutana na hali hii hata kama una uhakika kuwa mstaarabu. Tafuta muda wa kuongea naye hasa uso kwa uso na kama ikishindikana basi kwa simu. Muambie kuhusu maendeleo ya mtoto, acha kumzungumzia sana mke wake bali zungumzia mtoto, mfano muambie namna unaona mtoto hana afya, unahisi hali vizuri, muambie kuhusu makovu ya mtoto na namna maendeleo yake ya shule yalivyopungua.
Kama una ushahidi muonyeshe hata kama ni wa kuambiwa, muambie unaona mtoto hana furaha, muambie kile ulichokigundua ulipoongea na mtoto au ulichokiona. Narudia usilalamike, muambie na hata kama unahisi mkewe anamfanyia mambo flani basi muambie na muambie achunguze. Usimpe uamuzi hapohapo, labda ukamuambia nataka hivi na vile, nataka ufanye hivi na vile.
Hapana, hapo utakua unampangia na hatakusikilizi, muambie achunguze na anjaribu kuongea na mkewe ili kujua tatizo ni nini. Muambie ajaribu kuongea na mtoto kistaraabu bila kumtisha na kama kuna vitu vya kuona muambie amuangalie sehemu flani na flani na kama ni mtu wa kuuliza basi muambie muulize flani na flani. Hapo ni rahisi kukusikiliza na kukuelewa kuliko kumpangia na kumpa masharti siku ya kwanza.
(5) Shirikisha Ndugu/ Viongozi Wa Dini; Wanaume wengine washapikwa au viuno vimewachanganya na hawaoni, ukiwaambia wanakuona kama fala hawatafanyia kazi, hembu ukiona kimya hakuna mrejesho, usichukue hata wiki mbili au tatu, wiki tu ukishaongea naye ukaona hajali au kama ulishaongea na kuongea hembu tafuta ndugu. Kuna yule ndugu yake ambaye anamsikiliza zaidi.
Kuna yule mwenye busara hembu ongea naye muambie kila kitu ili aongee naye, lakini inawezekana ndugu zake huongei nao, wanakuchukia au yeye kwao ndiyo mwenye fedha hivyo ni kama vile wanamuabudu. Basi nenda kwa kiongozi wa dini naamini yupo, muambie ishu yako na muombe aingilie kati kwa kuongea na wa husika, hii itasaidia kuwaweka pamoja na hata kuona njia akabadilika.
(6) Nenda Ustawi Wa Jamii/Polisi; Wakakti mwingine kote huko hushindikana, una uhakika kuwa mwanao anateseka, una ushahidi na ushafanya kila kitu lakini bado wahusika hawajali acha kukaa kimya. Inawezekana mwanaume ana pesa, zaidi, huna kazi na hata akikuambia umchukue mwanao hutaweza kumlea lakini usikae kimya. Nenda Polisi, nenda ustawi wa jamii na mlinde mwanao.
Mumeo anaweza kuwa amelishwa limbwata, ndugu zake wanakuchukia na wasiwasikilize viongozi wa dini lakini kama Mama acha kuwa mnyonge na kusema namuachia Mungu wakati mwanao unaona anateseka, hapana, nenda Polisi, nenda ustawi wa jamii na hata huko ukikosa msaada nenda kwa Mkuu wa wilaya na hata Mahakamani.
Hatakama huendi kuwa unamchukua mwanao lakini nenda kuwa anateseka na unataka wahusika wa wajibike. Muhimu hapa ni kuhakikisha kuwa ananyanyasika, usiruhusu wivu ukaingilia maamuzi yako, usiruhusu chuki kwa huyo mwanamke mwingine ikaingilia maamuzi yako kwani Mahakamani, Polisi na ustawi wa jamii watahitaji ushahidi hivyo kama ushahidi wako ni wivu au chuki tu basi utampoteza na mwanao.