Mengi yamesemwa kuhusu kuwa mwanaume wa kweli, lakini ni machache yaliyosemwa kuhusu nani hasa mwanaume wa kweli. Mkazo mkubwa umekuwa ukiwekwa kwenye vitu vya juujuu, lakini mwanaume wa kweli hasa ni zaidi ya vitu hivyo.
Ni nani mwanaume wa kweli na hufanya nini?
MWANAUME WA KWELI HUWATENDEA WENGINE KWA HESHIMA
Mwanaume wa kweli ni mwenye heshima; huamiliana na wengine kwa heshima, wawe wanaume au wanawake. Sio mkaidi na mtovu wa heshima, na hamhehsimu mtu kwa kuangalia tabaka lake au hadhi yake ya kijamii.
ANAJUA TOFAUTI KATI YA KUJIAMINI NA KIBURI
Kuna msitari mwembamba unaotofautisha suala la KUJIAMINI na KIBURI, na wanaume wa kweli hawana kiburi, bali ni watu wanaojiamini na hawana nafasi ya kutojiamini.
ANA MOYO MWEMA
Mwanaume wa kweli ana moyo mwema; ni mtu mwema kwa watu wema.
ANAITHAMINI FAMILIA YAKE
Mwanaume wa kweli anaitambua thamani ya familia, anaipenda na kuienzi familia yake.
MWANAUME WA KWELI ANATHAMINI UHUSIANO
Mwanaume wa kweli ana thamini uhusiano wake na familia yake, uhusiano wake na marafiki zake na uhusiano wake na jamaa zake. Hufanya juhudi za kulinda na kuimarisha uhusiano wake na makundi mbalimbali.
ANATAMBUA THAMANI YA MUDA
Muda ni rasilimali ghali kabisa. Mwanaume wa kweli huthamini muda wake; anaelewa thamani ya muda na kuupangilia muda wake vizuri.
ANAKIRI MAKOSA
Mwanaume wa kweli ana mapungufu yake pia; anakiri makosa yake na kujifunza kutokana na makosa hayo.
Mwanaume wa kweli ni mkweli. Ni mtu ambaye unaweza kumuamini; si laghai na haishi maisha ya urongo.
Mwanaume wa kweli haishi tu, bali ana mwelekeo, malengo na mipango katika maisha yake.
Mwanaume wa kweli hashindani na watu wengine; hawahukumu watu wengine na haishi maisha ya kujilinganisha. Yeye ni yeye.
Mwanaume wa kweli ni mwenye kushukuru. Anawashukuru wengine kwa mazuri wanayomfanyia, hata kama ni madogo kiasi gani.
Mwanaume wa kweli hajazi chuki katika moyo wake, hashikamani na vinyongo au visasi dhidi ya watu wengine.
Linapokuja suala la familia yake, mwanaume wa kweli humpenda na kumpa heshima mkewe, ni baba ambaye ni mfano kwa watoto wake na ana mafungamano maalum na familia yake.
Mwanaume wa kweli hufanya kile anachohisi kuwa ni kitu kizuri chenye ubora, bila kujali kuwa wengine watamfikiriaje.
Mwanaume wa kweli hana manung’unike dhidi ya maisha, anapenda kuwa na furaha na anapenda kuwaona wengine wakiwa na furaha.