WAKATI mwingine hutokea. Unakuta umeachana na yule aliyekuwa anakusumbua na kukunyima furaha ila muda mfupi baadaye unahisi bado unamhitaji sana.
Unaanza kukumbuka zile nyakati njema mlizokuwa pamoja. Unamisi sura yake, umbile lake na kila kitu kizuri mlichofanya pamoja.
Katika hali ya ajabu unajikuta unasahau hata maudhi yake na kujikuta unakumbuka thamani na ubora wake.
Baada ya hapa unajikuta unatamani tena kuwa naye katika uhusiano kwa kuamini mambo yatakuwa safi na amani katika uhusiano wenu iliyokosekana kipindi kile itapatikana sasa.
Unajiaminisha kwamba mkiwa pamoja kila mmoja atakuwa kajifunza kosa lake na kujirekebisha.
Uko katika hali hiyo na mwenzako? Baada ya kugombana mara kadhaa na kuamua kuachana, umeanza kummisi na kuhitaji tena kuwa pamoja naye? Twende pamoja kujua uhalali wa wewe kurudiana naye.
Unakumbuka nini kilifanyika mkafikia uamuzi wa kuachana? Unakumbuka kabla ya kufikia hatua hiyo ni mara ngapi umejitahidi kumrekebisha ila imeshindikana?
Ni kawaida kumisi kitu ama mtu uliyeishi naye kwa muda mrefu. Kila binadamu wawili wanapokuwa pamoja kwa muda mrefu kunatengenezeka muunganiko wa ndani baina yao.
Muunganiko huu unawaunganisha wahusika kihisia, kifikra na hata kimaamuzi. Kwa sababu ya muunganiko huu, watu hata wakiwa mbali watakumbukana kwa muda fulani.
Ila kitu hiki huwa ni cha muda. Kama maji ambavyo ukiyatoa jikoni bado hubaki kuwa ya moto ila ukiyaacha chini kwa muda mrefu upo na kuwa baridi kabisa.
Ndivyo hali ya wahusika itakavyokuwa baadaye. Japo kwa muda fulani wanaweza kukumbukana kadiri wanavyokuwa mbali ndivyo ule muunganiko wao unavyozidi kupasuka.
Kama uliachana na mwenzako kwa sababu makini, kama kabla ya kuachana naye ulijaribu kumrekebisha na ikashindikana fahamu, hisia zako za kutaka kurudiana naye eti kwa imani ya kuwa atajirekebisha ni potofu.
Fikiria zaidi sababu zilizofanya mkaachana. Fikiria kero na maudhi aliyokufanyia yaliyokusukuma mkaachana.
Kufikiria mazuri yake baada ya kuachana naye ni tabia ya kujidanganya iliyofanya watu wengi warudiane na waliokuwa wakiwatesa na kuwaumiza na kujikuta wakipata mabalaa zaidi.
Wapo baadhi waliachana na wenzao na kwa pupa wakaanzisha mahusiano mengine. Kutokana na mahusiano husika walianzisha kwa pupa wakajikuta wapo na watu wanaowapenda ila wao bado wana fikra juu ya watu wao waliopita.
Bila kujua wanachofanya wakaamua tena kurudiana nao kwa imani kwamba wenzao watakuwa wamebadilika na kila kitu kitakuwa kama vile wanavyotamani kiwe.
Matokeo yake leo wanalia zaidi ya ilivyokuwa mwanzo. Maisha yako ni kitu muhimu sana kisichofaa kuchezewa kwa namna yoyote ile.
Kama unaamini uliachana na mwenzako kwa sababu makini na si kwa kukurupuka, usisikilize sauti inayokwambia eti mrudiane kwa sababu umemmisi ama kwa tumaini kwamba atabadilika.
Jiulize ni mara ngapi ulimpa nafasi ya kubadilika na hakufanya hivyo? Jiulize ni kwa muda gani ulivumilia mateso na kero zake kabla ya kuamua kuachana naye?
Mapenzi ni amani na furaha. Kama ulijitahidi kuvumilia changamoto na kero za mwenzako kwa tumaini la kupata raha na amani na bado hukupata, ni kwanini tena leo umuone anafaa?
Ni vema ukajua kutofautisha kati ya mazoea ya kuishi naye kwa muda mrefu na hitaji halisi la kuwa naye katika maisha yako kwa mara nyingine.
Wengi wanasumbuliwa na mazoea na kudhani bado wanahitaji waliokuwa wapenzi wao. Matokeo yake wakirudi wanajikuta katika awamu nyingine ya majuto na mateso makubwa.
Katika maisha kuna wakati inabidi ukubali kuumia kidogo ili uje kupata furaha ya kweli baadaye.
Kama ulimpima kwa vigezo halisi na kuona hafai na kuamua kuachana naye, kubali kuumizwa na mazoea kwa maana ni kitu cha muda mfupi na baadaye utakaa sawa.
Acha kusukumwa na hisia za kumkumbuka mwenzako na kuamua kumrudia hali unajua si mtu mwafaka kwako.
Kurudiana na mwenzako hali unajua si mwafaka kuna athari mbili. Kwanza unazidi kujiweka katika mahusiano ya kukera na kukuumiza ila pili unazidi kumfanya azidi kuzama katika akili yako na kuwa ngumu kuachana naye.
Kuna wakati mtu inabidi apoteze kitu kizuri alichozoea kwa ajili ya kitu kizuri kitakachompa faraja na raha.
Maisha ni kujifunza. Acha kupoteza muda kuwaza kurudiana na mtu asiyefaa badala yake chukulia yote yaliyotokea katika uhusiano wako kama elimu itakayokuongoza kukujenga na kukuimarisha katika maisha yako.
Hali ya maisha ya watu wengi imeharibika kwa kurudiana na walioachana nao hata kama walijua kuwa ni watu wa ovyo wasiojali na kuthamini.
Maisha yako kustawi yanahitaji uwe na mahusiano makini yenye kukupa amani na furaha kwa maana furaha ndio chanzo cha kukua kwa ubunifu na utulivu wa akili.
Ukiwa na mahusiano ya ovyo yatachangia kudumaza akili yako kwa sababu ya msongo wa mawazo. Muache aende kama uliamua kuachana naye kwa sababu sahihi.
Muache aende, maisha yako yanahitaji mtu makini ili uwe kufurahia na kuona raha ya dunia.